KILIMO KUWA CHANZO KIKUBWA PATO LA TAIFA
RUVUMA
Mhe.Rais Dkt Samia Suluhu Hassan amesema serikali inalenga kukifanya kilimo kuwa chanzo kikubwa cha kuchangia katika pato la taifa.
Akizungumza septemba 25 katika eneo la Litola Wilaya ya Namtumbo Mkoa wa Ruvuma Dkt Samia amesema kilimo kimekuwa sekta kubwa ya uzalishaji inayoiingizia serikali fedha kwa uharaka zaidi.
Aidha Mhe.Rais Samia amewahakikishia wananchi wa eneo hilo kuwa serikali itaendelea kuwaunga mkono katika sekta ya kilimo ikiwemo kutoa ruzuku mbalimbali.
“Kwa sasa serikali inatoa ruzuku ya mbolea, lakini pia nimemuagiza waziri aweke ruzuku ya mbegu, bei za mbegu zitashuka, kwasababu serikali itabeba nusu ya gharama yake,”amesema Rais Samia.
Katika hatua nyingine Kiongozi huyo wa nchi ameonya uchomaji moto mashambani kwani vitendo hivyo vinaharibu mazingira na misitu iliyohifadhiwa.
Vile vile Rais Samia amewataka wananchi wa wilaya hiyo kufanya kazi kwa bidii hasa katika sekta ya kilimo ili kuendelea kuchangia mapato.
