SERIKALI KUWAINUA WACHIMBAJI WADOGO WA MADINI
RUVUMA
Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan amesema serikali imeanzisha mikakati mbalimbali ya kusaidia wachimbaji wadogo na kuongeza mchango wa sekta ya madini katika uchumi wa taifa.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara septemba 26 wilayani Tunduru, Mkoa wa Ruvuma, katika siku yake ya nne ya ziara ya kikazi, Dkt Samia amesisitiza mikakati ya serikali ya kukuza sekta ya madini, hasa kwa kuwasaidia wachimbaji wadogo kupitia Dira ya 2030 ya sekta ya madini.
Katika ziara yake mkoani humo, Dkt Samia amezindua soko jipya la kisasa la madini, lililojengwa kupitia Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) kati ya Halmashauri ya eneo hilo na wafanyabiashara wa madini.
“Serikali kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) imetenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa mitambo 15 ya kuchimba visima, mitano kati ya hiyo tayari imetolewa ili kuwasaidia wachimbaji wadogo kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza ufanisi,” amesema Rais Samia.
Mitambo kumi iliyosalia inatarajiwa kuwasili hivi karibuni.
Jitihada hizi za serikali ya awamu ya sita zimechangia ukuaji wa kasi wa kila mwaka wa asilimia 10.9 katika sekta ya madini, ambayo sasa inachangia asilimia 9.1 kwenye Pato la Taifa la Tanzania.
