VIWANDA NA BIASHARA VYAWEKEWA MAZINGIRA WEZESHI
Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa ustawi wa viwanda na biashara nchini kwa kuandaa na kutekeleza sera, sheria, mikakati na miongozo mbalimbali.
Katika mwaka wa fedha 2023/2024, Serikali imefanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Biashara ya Mwaka 2003 na kuandaa Mkakati wa Taifa wa Utekelezaji Mkataba wa Soko Huru la Afrika.
Halikadhalika, Serikali imefanya marekebisho ya Sheria ya Leseni za Biashara na Kanuni zake, Sheria ya Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara, Sheria ya Wakala wa Vipimo na kufanya maboresho ya mfumo wa usajili kwa njia ya mtandao ili kurahisisha usajili.
Hatua hiyo imeboresha utoaji wa huduma na usimamizi wa shughuli za viwanda na biashara nchini na kuiwezesha Serikali kusajili Makampuni 8,523 kati ya 7,500 yaliyokusudiwa sawa na 114% na kutoa leseni za viwanda 118 kati ya 100 zilizokuwa zimepangwa sawa na 118%.
Vilevile, Serikali imeendelea kuratibu mradi wa maandalizi ya Kongani ya Viwanda ya Kwala ambapo hadi sasa ujenzi wa barabara kuu ya ndani, jengo la utawala, jengo la zimamoto,jengo la hosteli, majengo mawili ya viwanda na jengo la kufundishia mafundi umekamilika.