SERIKALI KUFUFUA, KUJENGA VIWANDA NCHINI

 

SERIKALI  KUFUFUA, KUJENGA VIWANDA NCHINI

SERIKALI  KUFUFUA, KUJENGA VIWANDA NCHINI

MOROGORO
Mhe Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema serikali inaendeleza na kutekeleza azma ya uanzishaji wa viwanda nchini ili kufikia ushindani na ukuaji wa uchumi.
Rais Samia amezindua mipango ya kuimarisha viwanda vya Morogoro na mikoa mingine, kwa lengo la kuboresha uchumi wa nchi, kuinua hali ya maisha ya watu, na kutengeneza fursa za ajira kwa vijana.
Akihutubia katika mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Jamhuri Manispaa ya Morogoro katika siku ya mwisho ya ziara yake ya siku sita mkoani humo, Rais Samia ameeleza maono yake ya sekta ya viwanda mkoani humo.
 “Naiona Morogoro kuwa kitovu cha viwanda, ikishindana na mikoa ya Pwani na Dar es Salaam ,Mpango huu umeundwa ili kuzalisha ajira kwa vijana na kuchochea ukuaji wa uchumi katika mkoa na taifa kwa ujumla,” amesema Rais Samia.
Ameongeza, “Nimemuagiza Waziri wa Viwanda na Biashara ahakikishe kuwa viwanda vyote vilivyokufa vinafufuliwa. Hata wakiamua kubadilisha kile walichokuwa wakizalisha awali, viwanda hivi lazima vianze tena kufanya kazi na kuendana na mahitaji mapya ya uzalishaji.
Dkt Samia ameongeza kuwa serikali pia inawekeza kwa kiasi kikubwa katika miundombinu ya usafirishaji, kama vile barabara na madaraja, ili kurahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa, na hivyo kuimarisha biashara ya ndani ya kikanda.
Aidha, Dk Samia amesema serikali imeanzisha vyuo vya ufundi stadi katika kila wilaya ili kuwapa vijana ujuzi wa kujiajiri na kuwaandaa kwa ajili ya fursa za baadaye katika viwanda vipya vilivyoanzishwa au kufufuliwa.