DKT SAMIA AZITAKA TAASISI ZA UMMA NA BINAFSI KUSHIRIKIANA
ARUSHA
Mhe Rais Dkt Samia amezitaka taasisi za umma kusaidia sekta binafsi katika kufikia masoko ya kimataifa.
Wito huo ameutoa Agosti 28 Mkoani Arusha wakati akifungua kongamano la Wenyeviti wa Bodi za Wakurugenzi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma huku akitolea mfano Hospitali ya Taifa Muhimbili jinsi inavyovuka mipaka kwa kuleta wataalam kutoka nje ya nchi na kubainisha kuwa taasisi za ndani kama vile Shirika la Viwango Tanzania (TBS) zinapaswa kuwasaidia wazalishaji wa ndani kufikia viwango vya kimataifa ili kuzuia uingizaji wa bidhaa zisizo na ubora.
Katika hatua nyingine Mhe. Rais Samia amezungumzia mageuzi yanayoendelea yanayolenga kuongeza tija katika taasisi za umma.
"Tumeanza mpango huu kwa sababu tuna mwongozo kutoka kwa Ilani ya CCM ya 2020-2025 kwamba Serikali inapaswa kuimarisha taasisi za umma ili ziendelee kuchangia maendeleo ya Taifa," amesema Dkt Samia.
Dkt Samia ameongeza “Mageuzi huleta tija, tusiwakatae. Wacha tubadilike kwa kasi yetu hadi tufike tunakoenda,”
Pia ametoa wito kuwe na mafunzo kwa Watendaji Wakuu kutoka sekta binafsi ili kuelewa utendaji wa serikali bila kuwekewa vikwazo na urasimu, na kuwahimiza kuleta mabadiliko katika sekta ya umma.
"Tuwape fursa na ushirikiano ili kuleta mabadiliko katika sekta ya umma," Dkt Samia amesema