BAKWATA KUMPATIA TUZO DKT SAMIA AGOSTI 31

 

BAKWATA KUMPATIA TUZO DKT SAMIA AGOSTI 31

BAKWATA KUMPATIA TUZO DKT SAMIA AGOSTI 31

DAR ES SALAAM
BARAZA la Waislamu Tanzania (BAKWATA), limetangaza kumpa tuzo Mhe Rais Dkt Samia, kama sehemu ya kutambua mchango wake katika kulitumikia Taifa.
Tuzo hiyo itatolewa Agosti 31, 2024 wakati Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan atakapohudhuria katika shindano la kusoma na kuhifadhi Quran kwa wanawake, linalotarajiwa kufanyika Agosti 31, 2024 .
Akizungumza na waandishi wa habari  jijini Dar es Salaam, Sheikhe Mkuu wa Tanzania, Dkt. Abubakar Zuber Bin Ally, amesema ni furaha kubwa kwa shindano hilo kuhudhuriwa na Mhe Rais, ikiwa ni mara ya kwanza kwa kiongozi huyo wa nchi kushiriki kama mgeni rasmi katika mashindano ya kusoma na kuhifadhi quran tangu alipoapishwa kushika wadhifa huo, Machi 2021.
“BAKWATA inamtangaza Rais Samia kama mgeni rasmi katika shindano hili la wanawake linalofanyika nchini kwetu kwa mara ya kwanza likishirikisha wanawake wa nchi 12 duniani, lenye dhumuni kubwa la kumuheshimisha mwanamke katika ulimwengu wa Quran.
“Pamoja na mambo mengine, siku hiyo kutatolewa tuzo kwenda kwa Rais Samia, sambamba na wale wote ambao kwa namna moja ama nyingine wana mchango mkubwa katika ukuzaji na utangazaji wa dini yetu ndani na nje ya nchi yetu,” alisema Mufti Zuber.
Katika hatua nyingine, Mhe.Rais Samia atashuhudia pia uzinduzi wa ‘Msahafu’ uliokuwa kwenye mfumo wa Eletroniki, kama njia ya kurahisisha usomaji wa Quran ulimwenguni, haswa kwa wakati huu Dunia inapiga hatua kubwa katika Sayansi na Teknolojia.