SERIKALI YAWALIPIA TSH BIL 5 WAGONJWA
DAR ES SALAAM
Serikali ya awamu ya sita chini ya Dkt Samia Suluhu Hassan imetoa shilingi bilioni 5 kwa hospitali tatu ili kulipia gharama za huduma maalum za matibabu zinazotolewa kwa wagonjwa ambao hawawezi kumudu gharama hizo.
Hospitali zilizopokea fedha hizo ni pamoja na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) na Hospitali ya Benjamin Mkapa ya Dodoma.
Kupitia ufadhili huo Jumla ya wagonjwa 28 wamenufaika wakiwemo watoto 16 waliowekewa mishipa ya fahamu, wagonjwa sita waliopandikizwa figo na sita waliopandikizwa uboho.
Aidha uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali katika sekta ya afya katika miundombinu ya utoaji wa huduma za afya, vifaa vya matibabu na vifaa pamoja na mafunzo ya wafanyakazi wa matibabu umewezesha upatikanaji wa huduma zote muhimu zikiwemo za kawaida, maalum na huduma za kitaalam nchini.
