DISEMBA 2024 DARAJA LA KIGONGO-BUSISI KUANZA KUTUMIKA

 

MWANZA

Daraja la J.P.Magufuli (Kigongo – Busisi) linalojengwa kwa gharama ya Shilingi Bilioni 592.6 bila 18% VAT ambalo lina urefu wa Kilomita 3.0 na barabara unganishi Kilomita 1.66 linatarajiwa kuanza kutumika tarehe 30 Disemba 2024 likiunganisha Barabara Kuu ya Usagara – Sengerema – Geita zenye urefu wa Kilomita 90.

Daraja hilo linajengwa Urefu wa kilometa 3.0 Upana meta 28.45 unaojumuisha njia mbili (2) za Magari (Carriageways) zenye upana wa meta 7.0 kila upande, njia ya maegesho ya dharura mita 2.5 kila upande, njia za watembea  kwa migu (Walkways) mita 2.5 kila upande, eneo la kati linalotenganisha  uelekeo tofauti wa barabara (Median) mita 2.45, kingo za magari (GuardRails Kerbs) meta 0.5 kila upande, na kingo za watembea kwa miguu (HandRails Kerbs) mita 0.5 kila upande.

Faida zitakazopatikana baada ya kukamilika kwa daraja hilo ni pamoja na kupunguza muda wa kusafiri na uwepo wa uhakika wa usafiri masaa 24, kuondoa msongamano wa magari uliokuwa unatokea kwenye feri, Litakuwa kiungo muhimu kwa Mkoa wa Mwanza na Mikoa inayouzunguka pamoja na Nchi  Jirani na pia daraja hilo litakuwa kivutio muhimu kwa Mkoa wa Mwanza na ni nembo kwa nchi ya Tanzania.

Aidha  Mradi huo umeshatoa jumla ya ajira 29,211 tangu kuanza kutekelezwa ambapo 93.33% sawa na ajira 27,262 ni Wazawa na ajira 1949 sawa na 6.67% ni Wageni.