MKUTANO WA G20 WAANZA KWA KISHINDO

 

MKUTANO WA G20 WAANZA KWA KISHINDO

MKUTANO WA G20 WAANZA KWA KISHINDO

BRAZIL 
MKUTANO wa 19 wa Viongozi kundi la G20 umeanza Novemba 18  Jumatatu mjini Rio De Jenairo Brazil ambapo ushiriki wa Tanzania unatajwa kusaidia kupata fedha za masharti nafuu, na ushirikiano kwa ajili ya kupanua upatikanaji wa nishati safi.
Mhe. Rais Dkt  Samia Suluhu Hassan tayari yuko Rio De Jenairo kushiriki katika mkutano huo wa kilele wa siku mbili na ushiriki wake unakuwa ni kwa mara ya  kwanza Tanzania kuhudhuria mkutano huo wa viongozi wa G20 tangu kupanuka kwa kundi hilo kutoka G8 hadi G20 mwaka 2009.
Umoja wa Afrika unashiriki katika mkutano huo kama mwanachama kwa mara ya kwanza tangu kukubaliwa kama mwanachama wa kundi hilo mnamo Septemba 2023.
Ushiriki wa Tanzania katika mkutano huo utasaidia juhudi za serikali katika mapambano dhidi ya umaskini na njaa pamoja na kufikia malengo ya maendeleo endelevu.
Mkutano huo utaipa Tanzania fursa ya kuvutia uwekezaji katika mipango ya usalama wa chakula kwa kukuza kilimo kinachozingatia hali ya hewa, kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi hususan kwenye mifumo ya chakula na kuimarisha ustahimilivu wa kikanda.
Ushiriki wa Rais Dkt Samia katika mkutano wa G20 unatarajiwa kuinua hadhi ya Watanzania katika ngazi ya dunia ili kukuza ushirikiano wa muda mrefu katika kufikia dira ya muda mrefu inayoendana na malengo ya maendeleo.
Aidha  mkutano wa viongozi wa G20 utajadili vipaumbele vya maendeleo endelevu ambavyo ni ushirikishwaji wa kijamii na mapambano dhidi ya njaa na umaskini, mabadiliko ya nishati sambamba na kukuza maendeleo endelevu katika nyanja zote za kiuchumi, kijamii na kimazingira.
FAHAMU:- G20 inaundwa na Argentina, Australia, Brazili, Canada, China, Ufaransa, Ujerumani, India, Indonesia, Italia, Japan, Mexico, Urusi, Saudi Arabia, Afrika Kusini, Korea Kusini, Uturuki, Uingereza na Marekani.