ASEMACHO DKT SAMIA ZIARANI KATAVI & RUKWA
RUKWA
Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan amesema amefurahishwa na miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika mikoa ya Katavi na Rukwa akisema inazingatia Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020-2025.
Mkuu wa Nchi ameyasema hayo julai 15, alipokuwa akizungumza na wananchi baada ya kuzindua Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi, ikiwa ni siku ya kwanza ya ziara yake ya kikazi ya siku tatu mkoani Rukwa.
Dkt Samia amesema katika ziara yake ya kikazi Mkoani Katavi, amejionea miradi yote ya maendeleo inatekelezwa vizuri, akisema hali hiyo inafanyika mkoani Rukwa pia
Rais Samia ameeleza kuridhishwa kwake na matumizi ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya miradi hiyo, hasa akielezea kufurahishwa kwake na ujenzi wa hospitali kubwa mkoani Rukwa, ambayo pia inatoa huduma bora kwa wananchi. “Nimeridhishwa na ujenzi wa hospitali kubwa, ambayo imewekwa vifaa vya kisasa.
Uwepo wa hospitali hii unatoa unafuu mkubwa kwa watu katika mkoa… Nimezungumza na baadhi ya wagonjwa na wanatambua ubora wa huduma wanazopata hapa,”
Aidha Dkt Samia amewataka madaktari, wauguzi na kada zote za afya kuitunza hospitali hiyo iliyojengwa kwa zaidi ya shilingi bilioni 5, huku akisisitiza kuwa wanatakiwa kuzingatia weledi, maadili na kuwa wazalendo kila wakati.