TANZANIA & CHINA KUIMARISHA DIPLOMASIA
BEIJING
Baada ya miaka 60 ya uhusiano wa kihistoria kati ya Tanzania na China, nchi hizo zimetangaza kuendelea kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia unaolenga kujenga ulimwengu bora, wenye maendeleo na usalama.
Uthibitisho huo umetolewa Mei 17, 2024 wakati wa mkutano wa pamoja mjini Beijing ambapo ulishirikisha wizara ya mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki ya Tanzania na Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi ambapo wizara hizo zilijadili ushirikiano wa siku zijazo baina ya nchi hizo mbili.
Kupitia mkutano huo Waziri Wang aliipongeza Tanzania kwa urafiki wake thabiti katika miongo sita iliyopita, akisema, imejipambanua kuwa rafiki katika hali ngumu na mbaya.
“Tanzania imekuwa rafiki wa China siku zote. Kwa China, miaka 60 ina maana kubwa katika uhusiano. Hatua inayofuata baada ya hii ni kuendeleza uhusiano huu katika enzi mpya ya kujenga dunia yenye mafanikio, haki na salama kwa watu wote,” amesema Wang.
Bw Wang amesisitiza nia ya China ya kuzidisha uaminifu wa kisiasa, kuimarisha uwiano wa kimkakati, na kupanua ushirikiano wa kivitendo chini ya mwongozo wa makubaliano yaliyofikiwa na wizara hizo mbili.
Pia ameshukuru uungwaji mkono wa muda mrefu wa Tanzania katika masuala yanayohusu maslahi makuu ya China huku akisisitiza dhamira ya China ya kuiunga mkono Tanzania katika kulinda mamlaka yake, usalama na maslahi yake ya maendeleo.
Bw Wang, ambae pia ni mjumbe wa Ofisi ya Kisiasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China, amezungumzia uwezekano wa kupanua ushirikiano katika maeneo muhimu kama vile biashara, miundombinu, usindikaji na utengenezaji, uchumi wa kidijitali, uchumi wa bluu na nishati.
