TANZANIA YAUNGANA NA WIPO
USWISI
Tanzania yaungana na nchi wanachama wa Shirika la Miliki Ubunifu Duniani (WIPO) kupitisha na kusaini Mkataba wa kihistoria wa kimataifa kuhusu Miliki Ubunifu, Rasilimali za Kijenetiki na Maarifa ya Jadi.
Mkataba huo unalenga kulinda haki za wenyeji asilia na jamii za kijadi katika kuhakikisha matumizi ya rasilimali za kijenetiki na maarifa ya jadi katika tafiti na vumbuzi yanaleta faida kwa jamii hizo.
Mkataba huo wa kihistoria na wa aina yake umejadiliwa kwa takribani miaka 25 na nchi wanachama wa WIPO kabla ya kupitishwa rasmi tarehe 24 Mei, 2024 katika Mkutano wa Kidiplomasia uliofanyika katika Makao Makuu ya Shirika hilo Jijini Geneva, Uswisi.
Mhe Dkt. Abdallah S. Possi, Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa na Mashirika ya Kimataifa Jijini Geneva ameongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano huo wa Kidiplomasia uliopitisha Mkataba tajwa, na kusaini Mkataba kwa upande wa Tanzania.
Mkataba huo utaanza kutumika rasmi siku 30 baada ya nchi 15 kuwasilisha nyaraka za uridhiwaji wa Mkataba huo katika Ofisi za WIPO.
