TANZANIA KINARA UHURU WA VYOMBO VYA HABARI EAC
DODOMA
Tanzania imeshika nafasi ya kwanza katika nchi zinazolinda uhuru wa vyombo vya habari kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa mwaka 2024, kwa mujibu wa ripoti mpya ya taasisi ya kimataifa ya Reporters Without Borders (RSF).
Ripoti hiyo iliyotolewa mei 3 inaonesha kuwa Tanzania imepanda kutoka nafasi ya 143 kwa mwaka 2023 hadi nafasi ya 97 kidunia mwaka huu.
Kupanda huko kwa nafasi 46 ndani ya mwaka mmoja kunatokana na mafanikio makubwa ya kuimarika kwa mazingira ya uhuru wa vyombo vya habari nchini Tanzania kulinganisha na nchi zote za Afrika.
Kwa kushika nafasi ya 97 kati ya nchi 180 duniani, Tanzania imekuwa kinara wa nchi zote za Afrika Mashariki kwa uhuru wa habari mwaka huu.
Tanzania iko vizuri kwenye uhuru wa habari mbele ya Kenya (102), Burundi (108), Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (123), Uganda (128), Sudani Kusini (136), Rwanda (144) na Somalia (145).
Utafiti wa RSF umeangalia masuala kadhaa muhimu, ikiwemo misingi ya kisheria, hali ya kiuchumi, hali ya kisiasa, usalama wa wanahabari na dhana ya kijamii na kitamaduni.
Tangu alipoingia madarakani Machi 2021, Rais Samia ameimarisha uhuru wa vyombo vya habari nchini kama sehemu ya Falsafa yake ya 4R.
KUMBUKA:- Jumanne Aprili 6, 2021 Dkt Samia alitoa agizo la kuiagiza iliyokuwa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kuvifungulia vyombo vya habari na kuwataka watendaji waepuke kuvishughulikia kwa namna ambayo inaweza kusababisha Serikali kulaumiwa kwa kuminya uhuru wa habari.
