ZIARA YA DKT SAMIA UTURUKI YAKUZA BIASHARA HADI TSH TRIL 2.5
DAR ES SALAAM
Tanzania na Uturuki zimekubaliana kukuza uhusiano baina ya nchi hizo mbili kwa kuongeza kiwango cha biashara kutoka dola za Marekani milioni 300 (zaidi ya bilioni 770) hadi dola bilioni 1 (zaidi ya trilioni 2.5/-).
Makubaliano hayo yamefanyika siku ya ijumaa (April 19) kupitia kongamano la lililowaleta pamoja wafanyabiashara 100 wa Kitanzania na wengine zaidi ya 200 kutoka Uturuki wakati Mhe Rais Dkt Samia akiwa ziarani Uturuki.
Akifungua kongamano hilo, Rais Samia Suluhu Hassan amewahimiza wawekezaji wa Uturuki kutumia fursa zilizopo katika nchi hiyo kubwa ya Afrika Mashariki, ikiwemo sekta ya kilimo, utalii na viwanda.
Dkt Samia alisema Tanzania ni eneo la kimkakati kama lango la ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini, ambalo linajumuisha soko la watu wapatao milioni 500.
Pamoja na njia za biashara zilizoimarika na mtandao wa bandari, ikiwamo Bandari ya Dar es Salaam kwenye Bahari ya Hindi, kuwekeza Tanzania kunamaanisha kupata fursa ya kupanua biashara na uwekezaji,” Rais Samia alisema.
Aidha Kufuatia ziara hiyo wakuu wa nchi (Tanzania na Uturuki) wameweka lengo la biashara la dola bilioni 1 (sawa na shilingi trilioni 2.5) ambazo zitapatikana baada ya utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa ikiwemo utekelezaji wa Mikataba sita ya Maelewano (MoUs) kuhusu elimu ya juu, diplomasia ya uchumi na ushirikiano wa kitamaduni.