TSH TRIL 3+ KULETA USHIRIKIANO MPYA TZ, UINGEREZA
DODOMA
SERIKALI ya Uingereza imezindua mfululizo wa ushirikiano mpya unaolenga kuimarisha maendeleo katika afya, uwekezaji wa kijamii na ukuaji wa uchumi shirikishi nchini Tanzania.
Miongoni mwa mipango iliyotangazwa ni ahadi ya kufungua ushirikiano huo kwa kutolewa kiasi cha takribani shilingi trilioni 3.260 katika uwekezaji unaoungwa mkono na serikali ya Tanzania.
Taarifa hiyo imetolewa jijini Dodoma na Waziri wa Nchi wa Uingereza anayeshughulikia Maendeleo na Afrika, Andrew Mitchell, wakati wa ufunguzi rasmi wa ofisi ndogo ya Ubalozi wa Uingereza.
Bw Mitchell amesisitiza kwamba msaada wa Uingereza umeongezeka mara tatu, huku mojawapo ya ushirikiano muhimu ukizingatia ajenda ya ustawi wa pande zote inayolenga kuchochea uwekezaji na biashara kwa ukuaji endelevu na kuunda nafasi za kazi.
Ubia huo unalenga kufungua uwekezaji unaofadhiliwa na serikali ya Uingereza nchini Tanzania ili kukuza biashara ya Uingereza na Tanzania kupitia uwekezaji katika Biashara Ndogo na za kati za Tanzania (SMEs)
Pamoja na hayo kiasi cha shilingi bilioni 48.932 kitatolewa kwa ajili ya kuimarisha zaidi mifumo ya afya kwa miaka mitano.
Uwekezaji huo utafanya kazi kwa ushirikiano na serikali ya Tanzania ili kuimarisha ustahimilivu wa huduma za afya, kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika, na kukabiliana na milipuko ya magonjwa, kusaidia safari ya nchi kuelekea Utoaji wa Huduma za Afya kwa Wote (UHC).
Aidha, serikali ya Uingereza itatenga dola za Marekani milioni 6.9 takriban bilioni 17.85 ili kuongeza nguvu kwenye miradi ya mabadiliko ya tabianchi na mazingira nchini Tanzania. Ufadhili huu utakuza teknolojia ya kupikia safi, ufikiaji wa nishati safi na ustahimilivu wa mijini, hadi 2026.
CHUKUA HII:- Uingereza imekuwa mwekezaji mkubwa nchini Tanzania, ikiwa na miradi 956, yenye thamani ya shilingi trilioni 14.994 na kuajiri zaidi ya watu 275,000, kuchangia uzalishaji wa ajira, maendeleo ya kiuchumi na maendeleo ya teknolojia, na mshirika wa muda mrefu katika kusaidia maendeleo ya Tanzania katika juhudi zake kwenye sekta mbalimbali.