TANZANIA YAAHIDI KUISAIDIA SOMALIA KATIKA USALAMA
DAR ES SALAAM
Tanzania imeahidi kuendelea kuisaidia Somalia katika nyanja mbalimbali zikiwemo za ulinzi na usalama ili kuhakikisha amani endelevu katika nchi hiyo mpya ya Afrika Mashariki.
Mhe Rais Samia Suluhu Hassan ametoa ahadi hiyo (Leo) April 27, 2024 katika Ikulu ya Dar es salaam mara baada ya kumpokea na kuzungumza na Rais wa Shirikisho la Jamhuri ya Somalia Mhe. Dkt. Hassan Sheikh Mohamud aliyekuja nchini kwa ziara ya kitaifa ya siku moja.
Akitoa taarifa mbele ya waandishi wa habari,Dkt Samia Suluhu Hassan amesema serikali ya Tanzania iko tayari kutoa mafunzo kwa Wasomali katika masuala ya ulinzi na maeneo mengine, ikiwemo afya na elimu.
Mbali na ulinzi, Dk Samia amesema nchi hizo mbili zimeanza safari ya kuimarisha ushirikiano katika sekta ya afya na elimu.
Kwa upande wake, Rais wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamud, ameishukuru serikali ya Tanzania kwa kusimama nao katika nyakati ngumu.
Ziara ya Mohamud nchini Tanzania ni ziara yake ya kwanza nchini na ni ya kwanza tangu Somalia ijiunge na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
