TANZANIA, UTURUKI KUKUZA BIASHARA, UWEKEZAJI
UTURUKI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania itaendelea kuimarisha uhusiano wa kiplomasia na kiuchumi ili kuleta ustawi zaidi katika mataifa hayo mawili.
Dkt Samia ameyasema hayo katika mkutano na waandishi wa habari pamoja na Rais wa Uturuki, Recep Tayyip ErdoÄŸan, Ikulu ya Ankara siku ya Alhamisi April 18,2024.
Wakati wa hafla hiyo, wakuu hao wawili wa nchi wameshuhudia utiaji saini wa Hati sita za Makubaliano (MoUs) ambazo zitarahisisha ushirikiano katika maeneo ya elimu ya juu, ushirikiano wa kiuchumi na kubadilishana utamaduni.
Akizungumza mbele ya waaandishi wa habari Mhe.Rais Samia amebainisha kuwa wamewaelekeza mawaziri wenye dhamana na timu zao za wataalamu kukutana na kuja na mkakati wa kuweka mikakati ya utekelezaji wa maeneo ya ushirikiano.
“Uturuki imekuwa mshirika wa thamani na Tanzania, hivyo basi, ziara yangu mjini Ankara inasisitiza kujitolea kwangu kuthamini ushirikiano huu,” amesema Dkt Samia
Kuhusu uhusiano uliopo baina ya nchi hizo, ameongeza kuwa umefungua njia kwa wataalamu wa Uturuki kuchangia katika kuleta mabadiliko ya Tanzania kupitia utekelezaji wa miradi mikubwa ikiwemo ya reli ya kisasa (SGR) inayounganisha Tanzania na nchi nyingine jirani.
“Kuhusu kukuza biashara na uwekezaji, Tanzania inalenga kushirikiana na sekta binafsi ya Uturuki, na tutakutana kesho (Leo April 19) Istanbul.
"Ushirikiano utazingatia jumbe tatu muhimu: kuwafahamisha juu ya athari chanya ambayo wawekezaji na wafanyabiashara wa Uturuki wanaleta katika nchi yetu, kuwasilisha mazingira ya biashara nchini Tanzania, na kuelezea nafasi ambayo Tanzania inaweza kutoa biashara. Tunawakaribisha wawekezaji wa Uturuki, hasa katika nyanja za viwanda, kilimo, na utalii,” Rais Samia ameongeza
