MHE RAIS SAMIA ACHANGIA TSH MIL 100 UJENZI WA KANISA ARUSHA
ARUSHA
Rais wa awamu ya sita wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan amechangia kiasi cha shilingi milioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa la Parokia ya Mtakatifu Karoli Lwanga lililopo Usa River Jimbo Kuu la Katoliki la Arusha.
Kwa niaba ya Mkuu wa Nchi Dkt Samia, ofisi ya mkuu wa mkoa wa Arusha imekabidhi kiasi hicho cha fedha huku ikisisitiza salaam kutoka kwa Mhe. Rais Dkt Samia kwamba “Rais Samia ametoa mchango wake katika kuleta maridhiano, kuunganisha na kujenga umoja wa kitaifa” taarifa kutoka ofisi ya mkuu wa mkoa imeeleza.
Aidha Parokia ya Mtakatifu Karoli Lwanga ilianzishwa mwaka 1975 na ilikuwa na kanisa lenye uwezo wa kuchukua waumini 600. Hata hivyo kutokana na ongezeko kubwa la idadi ya waumini, parokia iliamua kujenga kanisa lingine kubwa lenye uwezo wa kuchukua waabudu 2,500.
Kwa mujibu wa uongozi wa parokia hiyo, ujenzi wa jengo la kanisa hilo ulianza mwaka 2010 na kugharimu shilingi bilioni 2.7 hadi kukamilika kwake.
