BAKWATA IMARISHENI SHULE ZILIZO CHINI YENU - DKT SAMIA
DAR ES SALAAM
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan amewahimiza Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) kuimarisha shule zilizo chini yao ili ziwe mfano bora wa kuigwa katika jamii.
Mhe Rais Samia ametoa kauli hiyo wakati akihutubia kwenye baraza la Idd-El-Fitri lililofanyika katika ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNCC) Dar es Salaam tarehe 10 Aprili, 2024.
Dkt Samia amesema “Bakwata, niwasihi muendelee kuimarisha shule zilizo chini yenu ili ziwe mfano bora wa kuigwa, hakikisheni pia mnaendelea kuwalea wanafunzi kwenye mafunzo ya elimu ya dunia na akhera”
Pia Mhe Rais Samia ametumia jukwaa hilo kuwakumbusha wamiliki wa shule za dini na za binafsi kuipa serikali ushirikiano ili kuleta tija kuendana na utekelezaji wa mabadiliko ya sera ya elimu “Nirudie kuomba ushirikiano kutoka kwenye taaisi za dini zenye shule pamoja na wamiliki wengine wenye shule binafsi ili kuhakikisha stadi zinazotolewa zinasadifu malengo ya sera ya serikali”Amesema Rais Samia.
Vilevile Dkt Samia amezungumzia kuhusu suala la mahitaji ya mabadiliko ya sera ya elimu kulingana na muuundo na mahitaji ya sasa kidunia na kubainisha kwamba kutokana na mahitaji hayo serikali iliamua kupitia sera ya elimu na mitaala ya elimu na mafunzo zoezi ambalo lilikamilika mwaka 2023 na mitaala na sera ya elimu na mafunzo toleo la mwaka 2023 limeanza kutumika kuanzia mwezi Januari 2024