ZIARA YA WMKUU WA ETHIOPIA NCHINI INA FAIDA GANI KIUCHUMI
DAR ES SALAAM
Siku za hivi karibuni Tanzania ilipata ugeni kutoka nchini Ethiopia Waziri Mkuu wa nchi hiyo Abiy Ahmed alipofana ziara ya kiserikali ya siku tatu kati ya tarehe 29 Februari hadi 2 Machi 2024
Ziara ya kiongozi huyo kutoka nchini Ethiopia ilikuwa na dhima ya kuimarisha ushirikiano wa kiusalama na kiuchumi kati ya nchi hizo mbili, hii ni kwa mujibu wa wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Pia kama nchi tumeshuhudia mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na waziri mkuu huyo wa Ethiopia hafla ya utiaji saini kwa mikataba kadhaa ya maelewano yenye lengo la kuimarisha uhusiano wa kibiashara zikiwemo kilimo, nishati biashara na ushirikiano wa kitamaduni.
Ethiopia inasifika kimataifa kwa uzalishaji wa kahawa na chai, chai na kahawa ya Tanzania ni maarufu, kwa hivyo, jinsi ya kupata masoko kwa pamoja itakuwa sehemu muhimu ya makubaliano ya nchi mbili wakati wa ziara hii. Ni muhimu tushirikiane ili kufikia masoko haya ipasavyo
Aidha ziara ya Bw Ahmed imekuwa ni jukwaa la kubadilishana uzoefu katika sekta ya mifugo ikizingatiwa kuwa Ethiopia imeshika nafasi ya kwanza kwa kuwa na idadi kubwa ya ng'ombe, huku Tanzania ikishika nafasi ya tatu.
Ushirikiano huu unaweza kusababisha ongezeko la kiwango cha biashara kati ya nchi hizo mbili. Tanzania pia inatarajia kuvutia Uwekezaji wa Moja kwa Moja wa Kigeni (FDIs) kutoka Ethiopia
Nchi hizo mbili zimetumia jukwaa hilo kuimarisha juhudi za kuhimiza amani, usalama na kukomesha biashara haramu ya binadamu inayohusisha raia wa Ethiopia ambao wamekuwa wakisafirishwa kwenda nchi nyingine kupitia Tanzania.
WACHAMBUZI WANA MATUMAINI KUWA ZIARA YA MHE AHMED ITAPANUA UHUSIANO KATI YA MATAIFA HAYO MAWILI, HASA KATIKA MAENEO YENYE MASLAHI YA PAMOJA.
Rais wa Chama cha Wahasibu Tanzania (TAA) Bw. Godvictor Lyimo, amesisitiza manufaa ya kiuchumi yanayoweza kupatikana kwa Tanzania, hususan katika sekta ya usafiri wa anga.
Bwan Godvictor amebainisha kuwa ziara hiyo ni fursa kwa Tanzania kupata maarifa kutokana na uzoefu wa Ethiopia katika kusimamia miradi mikubwa ya umeme wa maji, kama vile Bwawa la Grand Ethiopian Renaissance (GERD).
Amesisitiza uwezekano wa uhamisho wa ujuzi kati ya mataifa hayo mawili, hasa kuhusu ufanisi wa uendeshaji na matengenezo ya miradi hiyo.
Aidha Bw Lyimo ameeleza umuhimu wa ushirikiano katika sekta ya maji, kutokana na muunganiko wa rasilimali za maji kati ya nchi hizo mbili, hususan Mto White Nile, unaotoa maji kutoka Ziwa Victoria nchini Tanzania.
Nae Meneja Uhusiano wa Umma na Mhadhiri wa Kituo cha Mahusiano ya Kigeni (CFR) Bw Innocent Shoo, ameangazia uhusiano wa kihistoria na kidiplomasia uliokita mizizi kati ya Tanzania na Ethiopia, ulioanzishwa na viongozi kama vile Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Haile Selassie wa Ethiopia.
Bw Shoo amesisitiza ukuaji na kuimarika kwa sekta mbalimbali ambapo Tanzania na Ethiopia zina maslahi sawa, ikiwa ni pamoja na kilimo cha mifugo, uzalishaji wa mazao, umeme, viwanda vya nguo na anga.
#DIPLOMASIAINALIPA
