UCHAMBUZI- KUANZA UZALISHAJI JNHPP, WACHAMBUZI WANASEMAJE
DAR ES SALAAM
Wachambuzi na wadau wa maendeleo nchini wameonesha matumaini yao kufuatia kuanza kwa uzalishaji wa umeme katika Mradi wa Umeme wa Maji wa Julius Nyerere (JNHPP), wakisema kuwa maendeleo hayo mapya yatarahisisha shughuli za kiuchumi na kuinua zaidi hali ya maisha ya watu.
Maoni ya Wachambuzi hao yamekuja baada ya serikali kuthibitisha kwamba uhaba wa umeme, ambao umesababisha mgawo wa sasa, utaisha kabisa mwezi ujao kwani JNHPP imeanza kuingiza umeme kwenye gridi ya taifa.
Mradi huo hadi sasa umeingiza megawati 235 kwenye gridi ya taifa kutoka kwa turbine ya kwanza, ambayo kwa mujibu wa ratiba ilitakiwa kuanza Juni, mwaka huu.
NENO LA WACHAMBUZI KUHUSU HATUA ILIYOFIKIWA.
Mhadhiri wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Prof Humphrey Moshi anasema kuongezeka kwa uzalishaji wa umeme kupitia JNHPP kutaongeza kasi ya uzalishaji wa bidhaa mbalimbali nchini katika viwanda vidogo na vikubwa.
"Uzalishaji wa umeme katika JNHPP utaharakisha shughuli za uzalishaji nchini na kupunguza mfumuko wa bei za bidhaa, hivyo kuboresha ustawi wa watu," Prof Moshi amesema.
Prof Moshi ameongeza kamba kupitia bwawa la Nyerere, dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kukaribisha uwekezaji nchini sasa inatimia kwa sababu uwekezaji unakwenda pamoja na matumizi ya umeme katika uzalishaji.
Amesisitiza maendeleo hayo mapya yameifanya serikali kupata imani kwa wananchi kwa sababu iliahidi kuwa mradi huo unaweza kuanza kufanya kazi kuanzia mwaka huu na kutatua changamoto ya umeme nchini.
Mchangiaji mwingine wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Dkt Paul Loisulie amesema, kuanza kwa operesheni hiyo kutaongeza kasi ya shughuli za kiuchumi kwa kupunguza gharama za uzalishaji.
“Wananchi watakuwa na umeme wa uhakika katika shughuli za uzalishaji na pia kupunguza gharama za uzalishaji, sasa watatumia umeme ambao ni wa bei nafuu kuliko jenereta,” Dkt Loisulie amesema.
Dkt Ahmad Sovu Mchambuzi/mhadhiri wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, amesema, upatikanaji wa umeme wa uhakika utachochea uzalishaji hasa kwa wajasiriamali na wakulima nchini.
"Wakulima waliokuwa wakikamua mawese na mafuta ya alizeti ndani ya nchi sasa watatumia mashine na kupata mafuta bora,umeme wa uhakika ndio msingi wa uwekezaji kwa sababu maeneo ya uwekezaji yapo, lakini changamoto ni uhaba wa umeme, lakini sasa uwekezaji zaidi utakuja.
Dkt Sovu ameongeza kuwa serikali imejiweka imara kwa kutekeleza ahadi na kuthibitisha kuwa inajali na kutatua changamoto za wananchi.
