MRADI WA JOTOARDHI TANZANIA MBIONI KUANZA

 

MRADI WA JOTOARDHI  TANZANIA MBIONI KUANZA

MRADI WA JOTOARDHI  TANZANIA MBIONI KUANZA

KENYA
Tanzania itaanza kuchimba visima vya jotoardhi ili kujua rasilimali ya jotoardhi iliyopo kabla ya kuanza uzalishaji wa umeme, hii ni kwa mujibu wa wizara ya nishati nchini Tanzania ilipotembelea vyanzo na mitambo ya nishati ya jotoardhi katika Mji wa Naivasha, Kaunti ya Nakuru nchini Kenya.
"Tumetembelea mitambo ya nishati ya jotoardhi inayomilikiwa na Kampuni ya Kuzalisha Umeme ya Kenya (KenGen) na tumeona maendeleo waliyofanya katika kuendeleza rasilimali hii, kwani kwa sasa wanazalisha zaidi ya megawati 799 za nishati ya jotoardhi," Imesema wizara ya nishati ya Tanzania.
Taarifa ya wizara imeongeza kwamba Tanzania tayari imetenga fedha kwa ajili ya kuendeleza jotoardhi na kwamba kuanzia mwezi April kampuni ya KenGen itakuwa Mkoani Mbeya kuanza uchimbaji wa vyanzo vya jotoardhi katika eneo la Ngozi na Kiejo-Mbaka kwa kushirikiana na Kampuni ya Maendeleo ya Jotoardhi Tanzania (TGDC).
Aidha Tanzania inaelekeza nguvu zake katika kuongeza vyanzo vyake vya kuzalisha umeme, huku msisitizo ukiwa ni kuendeleza miradi ya jotoardhi ili kukidhi mahitaji ya nishati kwa wananchi.
Kwa upande wake Meneja Mkuu wa Maendeleo ya Jotoardhi KenGen  Peketsa Mangi amesema Kenya itatoa ushirikiano mzuri kati ya Kenya na Tanzania katika kuendeleza maendeleo ya jotoardhi.
Pia ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuiruhusu KenGen kufanya kazi na wataalam wa TGDC katika uchimbaji wa visima ili kutathmini rasilimali ya jotoardhi nchini, na kusema kuwa kampuni hiyo iko tayari kufanya kazi zinazohitajika kwa ufanisi.