WB KUPIGA JEKI TSH BIL 687 UBORESHAJI TAZARA
DAR ES SALAAM.
BENKI ya Dunia imeidhinisha ruzuku ya dola za Marekani milioni 270 takriban bilioni 687 za Kitanzania kusaidia uboreshaji wa mawasiliano ya usafiri na biashara kati ya Zambia na Tanzania(TAZARA).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Benki ya Dunia inasema fedha hizo zitatumika kukarabati sehemu ya TAZARA nchini Zambia, kuendeleza kituo cha kisasa cha mpaka kati ya Zambia na Tanzania na kuanzisha miundombinu mingine inayosaidia.
Taarifa hiyo inafafanua kuwa mradi wa miaka sita wa Njia za Kuhimili Kiuchumi (TRACER) unaoungwa mkono na Shirika la Maendeleo la Kimataifa (1DA) unalenga kuboresha ufanisi, uunganishaji, na ustahimilivu wa hali ya hewa wa njia kuu za uchukuzi na biashara za kikanda katika Mashariki na Kusini mwa Afrika.
Aidha mradi huo ni utekelezaji wa moja ya ajenda wakati Mhe Rais Samia Suluhu Hassan alipotembelea Zambia mwaka jana (2022).