TANZANIA YAONDOLEWA KWENYE ORODHA YA MADENI MAKUBWA
WASHINGTON, D.C.
Tanzania imeanza vizuri mwaka 2024 baada ya kuondolewa kwenye orodha ya nchi zenye madeni makubwa Afrika, hii ni kwa mujibu wa taarifa ya Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF) iliyotoa orodha ya nchi 10 zenye madeni makubwa Afrika, ambayo ilisema kitendo hicho cha Tanzania kuondolewa kwenye orodha hiyo kimetokana na kufanya vizuri kiuchumi na usimamizi mzuri wa fedha.
“Inaweza kuwa ishara nzuri na chanya kwa wawekezaji na taasisi za kifedha za kimataifa kwani inaashiria kuwa kiwango cha madeni cha Tanzania kinadhibitika kulinganisha na nchi nyingine katika ukanda wake,” inasomeka taarifa hiyo.
Taarifa hiyo inasema hali ya Tanzania kuondolewa kwenye orodha hiyo itaongeza hali ya kujiamini na kuvutia wawekezaji zaidi jambo ambalo ni muhimu katika kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Kenya ina deni la Dola za Marekani zaidi ya bilioni mbili, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ina deni la Dola za Marekani bilioni 1.29, Morocco Dola bilioni 1.499, Nigeria Dola bilioni 1.8.
Misri ina deni la Dola za Marekani bilioni 11.96, Angola bilioni 3.1, Afrika Kusini bilioni 2.66, Ivory Coast bilioni 2.1, Tunisia bilioni 1.2.
Kwa mujibu wa Wizara ya Fedha Nchini , deni la Serikali hadi Aprili 2023, lilikuwa Sh trilioni 79.10, sawa na ongezeko la 13.9% ikilinganishwa na Sh trilioni 69.44 Aprili 2022.
Aidha katika bajeti ya 2023/24 mikopo nafuu imeongezeka kwa 22.8% na yenye masharti ya kibiashara imepungua kwa 14.4%
KUMBUKA:- Mara kadhaa Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza kuwa nchi itakopa kwa kuangalia njia rahisi zitakazofaa.
“Kwa vyovyote vile tutakopa, tutaangalia njia rahisi zitakazotufaa kukopa kwa maana fedha hizi hatutazitoa kwenye kodi tunazokusanya ndani,” alisema Dkt Samia akizungumzia ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), Ikulu Dar es Salaam mwaka 2021.
