RAIS SAMIA AKITA MIZIZI KUHUSU KILIMO ENDELEVU

 

RAIS SAMIA AKITA MIZIZI KUHUSU KILIMO ENDELEVU

RAIS SAMIA AKITA MIZIZI KUHUSU KILIMO ENDELEVU

OSLO, NORWAY
Rais  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa mataifa ya Afrika kuharakisha kipindi cha mpito cha kuelekea kwenye kilimo endelevu ili kukabiliana na changamoto ya kulisha idadi ya watu inayoongezeka kwa kasi barani humo.
Akizungumza katika Mkutano wa Usalama wa Chakula na Ushirikiano wa Mabadiliko ya Tabianchi Oslo  Nchini  Norway wakati wa Ziara yake ya Kiserikali ya siku mbili Rais Samia amesisitiza uharaka wa kufuata kanuni za kilimo bora na zenye ufanisi zaidi ili kushughulikia upatikanaji wa usalama wa chakula wa barani Afrika.
Dk Samia ameangazia kazi kubwa ya Afrika ya kulisha watu kutokana na ongezeko la idadi, kufanya juhudi shirikishi, uvumbuzi, na utekelezaji wa mikakati inayoweka kipaumbele kukidhi mahitaji ya kizazi cha sasa bila kuathiri mahitaji ya vizazi vijavyo.
"Ni muhimu kwamba tushirikiane, kubuni, na kutekeleza mikakati ambayo inatusaidia kukidhi mahitaji ya kizazi cha sasa bila kuweka hatarini mahitaji ya vizazi vijavyo," Amesema Dkt Samia.
Aidha, Mhe Rais amesisitiza umuhimu wa siyo tu kuongeza uzalishaji wa chakula bali pia kutengeneza fursa za ajira na kuzalisha kipato kwa wakazi wa vijijini na mijini kupitia mifumo endelevu na yenye usawa ya uzalishaji na minyororo ya thamani.
Kwa kuzingatia dhamira ya Tanzania ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi na kuimarisha usalama wa chakula, Rais Samia alisisitiza kujitolea kwake kufanya kazi na jumuiya ya kimataifa kushughulikia masuala haya muhimu ndani na nje ya nchi.
Tanzania imejiwekea malengo makubwa, ikiwa ni pamoja na kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi kwa asilimia 30-35 katika uchumi mzima ifikapo mwaka 2030. Katika ziara yake, Rais Samia alishuhudia utiaji saini wa mikataba yenye lengo la kuimarisha ushirikiano baina ya Norway na Tanzania katika masuala ya usalama wa chakula na kilimo.
Mikataba hiyo ni pamoja na mashirikiano kati ya taasisi za Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) na Chuo Kikuu cha Sayansi ya Maisha cha Norway, pamoja na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) na Taasisi ya Utafiti wa Bioeconomy ya Norway.
Rais Samia pia ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kushirikiana katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi ambayo yanazidisha uhaba wa chakula hasa katika nchi za Afrika.