DKT SAMIA APIGIA DEBE MAGEUZI YA KIUCHUMI
ETHIOPIA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan ameeleza kuwa kukamilisha ukombozi wa kisiasa na mageuzi ya kiuchumi katika nchi za Afrika ni muhimu kwa mustakabali wa bara hili kuwa salama.
Mhe Rais Samia ametoa kauli hiyo februari 18 (Jumapili) kando ya Mkutano wa 37 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika wakati wa uzinduzi wa sanamu ya muasisi wa Tanzania Hayati Julius Nyerere katika Ofisi za Umoja wa Afrika (AU) mjini Addis Ababa, Ethiopia, akitoa wito kwa Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA),makubaliano ya kuchukua nafasi muhimu katika kuhakikisha ustawi na utu wa watu wa Afrika.
Mkutano huo pia umeheshimu mchango wa Nyerere katika Ukombozi wa Nchi za Kusini mwa Afrika na kukuza amani na usalama barani Afrika.
“Ni matumaini yangu kuwa kumbukumbu ya Mwalimu Julius Nyerere itahamasisha vizazi vya sasa na vijavyo kuwasha mienge yao wenyewe katika kutafuta matumaini, upendo na utu pale ambapo hakuna,” Amesema Rais Samia.
Dkt Samia ameongeza kwamba sanamu ya Mwalimu Nyerere ni kutambua mchango wake katika ukombozi, umoja na amani ya Afrika na kudhihirisha fahari katika urithi wa Afrika. Katika hatua nyingine, Mkuu wa Nchi ametoa shukurani zake kwa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) kwa kutekeleza mradi huo na AU kwa kutoa nafasi kwa sanamu ya Nyerere, pamoja na viongozi wengine wakubwa wa Kiafrika wakiwemo Haile Selassie na Kwame Nkrumah.
Aidha Rais Samia alinukuu maneno ya Nyerere wakati wa Siku ya Uhuru wa nchi, akisema: “Tumeongoza mwenge wa uhuru kuuweka katika kilele cha Mlima Kilimanjaro uangaze ndani na nje ya mipaka yetu ili kuleta matumaini pale penye kukata tamaa, upendo palipo na chuki na heshima palipo na dharau”
