WANANCHI WA MPIGAMITI WAISHUKURU SERIKALI KUWAFIKISHIA UMEME
LINDI
Wananchi wa Kijiji cha Mpigamiti Kata ya Mpigamiti Halmashauri ya Wilaya Liwale Mkoani Lindi, wameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Dkt Samia Suluhu Hassna kwa kuwapelekea huduma ya Umeme kwa kuwa hapo awali walilazimika kutembea Umbali wa Km 50 kwenda na kurudi Liwale mjini kufuata huduma zinazotegemea Nishati hiyo muhimu.
Bi Asuna Mohammed Mkabila mkazi wa Kijiji cha Mpigamiti B amesema pamoja na kuepuka kutembea umbali huo mrefu kufuata huduma hiyo, Lakini pia fursa nyingi za biashara zitafunguka kama vile kuuza Vinywaji baridi, kuanzishwa kwa Viwanda Vidogo na vitu vigine.
Nae Bw.Chande Halidi mkazi wa Kijiji hicho ameishukuru Serikali kwa kuwapelekea Ukombozi kwani Vijana wamechangamkia fursa kwa kuweka Mashine ya kusaga hivyo huduma hiyo inapatikana
hapohapo Kijijini.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Kijiji cha Mpigamiti Ndugu Sadiki Tewele amemshukuru Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwapa huduma hiyo kwa kuwa hawakuwaza kama na wao watafikiwa.
"Uwepo wa Umeme Kijijini kwetu umeleta maendeleo sio tu kibiashara lakini hata kwenye upande wa Maji tumenufaika maana wanafunga Mota zinazotumia Umeme, na Maji yatashuka, pili kuwa Mashine ya kusaga, kuna Viwanda vidogovidogo Kwahiyo tunamshukuru pia Mbunge wetu Zuberi Kuchauka kwa kutupambania Wananchi wake” amesema Tewele.
