OSAKA EXPO KUKUZA UTALII,UWEKEZAJI NCHINI
DODOMA
TANZANIA ni miongoni mwa nchi zaidi ya 160 zilizothibitishwa kushiriki Maonesho ya 2025, yanayotarajiwa kufanyika Osaka, Japan, kuanzia Aprili 12, mwaka huu ambayo yatahusu biashara, uwekezaji na utalii.
Maonyesho ya 2025 yanatarajiwa kuvutia zaidi ya wageni milioni 28.2 kutoka kote ulimwenguni
ambapo Tanzania itatumia hafla hiyo ya miezi sita inayoanza Aprili 12, kama fursa ya kuunganisha uzalishaji wa ndani na masoko ya kimataifa, kukuza uwekezaji kwa ubia, kukuza mawasiliano kati ya watu, bidhaa na teknolojia, kuchochea maendeleo ya miundombinu na kukuza utalii.
Aidha ushiriki wa Tanzania katika maonesho hayo ya kimataifa utazingatia sekta kama vile afya, nishati, madini, utalii, kilimo, uchumi wa bluu, sanaa na utamaduni, uwekezaji na biashara.
Serikali pia inakusudia kuonyesha miradi muhimu ya miundombinu, ikiwa ni pamoja na barabara, reli, viwanja vya ndege, bandari, umeme, gesi na mipango ya uchumi wa bluu.
Tanzania inatazamiwa kutuma zaidi ya washiriki 500 kutoka sekta mbalimbali, huku 170 wakiwa tayari wamesajiliwa kwa ajili ya Maonesho ya 2025 huko Osaka.
MUHIMU:- Ushiriki wa Tanzania katika Maonesho ya 2025 unaratibiwa na Wizara ya Viwanda na Biashara (Bara), kwa kushirikiana na Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda (Zanzibar), Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, na TANTRADE, chini ya mamlaka ya Sheria namba 4 ya mwaka 2009, iliyorekebishwa mwaka 2023.