TSH TRIL 57.04 KUENDELEZA MAGEUZI YA UCHUMI NCHINI
TANZANIA
SERIKALI inatarajia kukusanya na kutumia jumla ya shilingi trilioni 57.04 katika Mwaka wa Fedha wa 2025/26, nyongeza ambayo ni sawa na asilimia 13.4 ikilinganishwa na trilioni 50.291/ ambayo iliidhinishwa na wabunge kwa Mwaka wa Fedha 2024/25.
Fedha hizo, kwa mujibu wa serikali, zitatumika vyema katika maeneo matano ya kipaumbele yanayoendelea, kulingana na Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2020/21-2025/26) unaofikia kilele mwishoni mwa mwaka huu huku serikali ikijipanga kikamilifu kuhakikisha utekelezaji wa bajeti ijayo unaendelea kwa kuzingatia vipaumbele vyote katika jitihada za kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025.
Vipaumbele hivyo ni pamoja na kuchochea uchumi jumuishi na shirikishi, kuimarisha uzalishaji na utoaji wa huduma viwandani, kukuza biashara na uwekezaji, kuendeleza uchumi wa watu pamoja na kuendeleza rasilimali watu.
Kiasi hicho cha shilingi tril 57.04 zitatumika kulipa mishahara na marupurupu mengine ya kisheria kwa watumishi wa umma katika Serikali kuu ambayo yanatarajiwa kugharimu 7.7tril/-, manunuzi ya huduma na bidhaa (7.8tril/-) na fedha zitakazotolewa kwa Idara na Mamlaka za Wizara (MDAs) pamoja na Serikali za Mitaa.
Aidha, serikali ina mpango wa kununua mali kwa ajili ya taasisi mbalimbali za Serikali ikiwa ni pamoja na vifaa vya ofisi, mashine, magari, samani, ujenzi wa majengo na miundombinu (trili 3.03/-).