SERIKALI YATOA LESENI KUBWA YA MADINI KWA ECOGRAF
MOROGORO
Serikali imetoa Leseni Kubwa ya Uchimbaji (Special Mining Lisence- SML) kwa Kampuni ya EcoGraf Limited kupitia Mgodi wa Epanko Graphite, uliopo Kijiji cha Epanko Wilaya ya Mahenge, Mkoani Morogoro.
Hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa muda mrefu wa Serikali wa kuboresha Sekta ya Madini hapa nchini sambamba na kuongeza thamani kwa maliasili zake ikiwemo za madini ambako Mradi huo unatarajiwa kuleta mapinduzi makubwa katika uchumi, viwanda, ajira, na nafasi ya Tanzania katika soko la kimataifa la nishati safi.
Kabla ya hatua hii, Serikali ya Tanzania ilifanya tathmini ya kina ya maendeleo ya Mradi wa Epanko na kwamba Kampuni hiyo inatoa shukraniza dhati kwa Rais wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuidhinisha utolewaji wa leseni hiyo.
Serikali ya Tanzania itanufaika na kodi na tozo mbalimbali zitakazotokana na shughuli za mgodi wa Epanko ambapo mapato hayo yanaweza kuelekezwa katika miradi ya maendeleo kama vile ujenzi wa shule, hospitali, barabara, na miradi mingine ya kijamii.
Aidha jumla ya dola milioni 850 sawa na shilingi trilioni 2.1 zinazotarajiwa kulipwa na kampuni hiyo kama kodi, gawio, ada, mrabaha na ununuzi wa huduma na bidhaa tofauti katika kipindi cha kuendesha shughuli zake, inakadiriwa itachangia zaidi ya dola bilioni 2.5 sawa na shilingi trilioni 5.6 kwenye pato la Taifa (GDP).