WANAFUNZI 974,332 KUJIUNGA KIDATO CHA KWANZA 2025
DAR ES SALAAM
Waziri wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR - TAMISEMI) Mohamed Mchengerwa ametangaza jumla ya wanafunzi 974,332 waliofaulu mitihani ya darasa la saba mwaka 2024 watapata nafasi ya kujiunga na kidato cha kwanza Januari 2025 kwa mkupuo mmoja ( Bila uwepo wa chaguo la pili) hii ni kutokana na uwekezaji wa miundombinu ya kutosha kwenye sekta ya elimu iliyofanywa na serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.
Waziri Mchengerwa ametoa taarifa hiyo leo Desemba 16, 2024 wakati akizungumza na vyombo vya habari Jijini Dar es salaam ambapo amesema
“Jumla ya wanafuni 974,332 sawa na asilimia 100 ya wanafunzi wote waliokuwa na sifa ya kuchaguliwa wakiwemo wasichana 525,225 na wavulana 449,107, wenye sifa ya kujiunga na kidato cha kwanza watapata nafasi ya kujiunga na kidato cha kwanza bila kuwepo kwa chaguo la pili kama ilivyokuwa huko nyuma”
Kufuatia hatua hizi za mageuzi haya makubwa katika sekta ya elimu, Waziri Mchengerwa amempongea Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan
“Ninamshukuru Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza katika sekta ya elimu kwa kuhakikisha kila mtoto wa kiTanzania anapata fursa ya kupata elimu”Amesema Mhe. Mchengerwa.
Aidha uchaguzi wa wanafunzi wa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2025 umezingatia kigezo cha ufaulu wa mtahiniwa anaechaguliwa ambapo kila mtahiniwa aliyefanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka 2024 na kupata jumla ya alama ya ufaulu kati ya 121 hadi 300 amechaguliwa na kupangiwa shule ya sekondari ya serikali.
