TSH BIL 323 KUTEKELEZA MIRADI YA MAENDELEO
DAR ES SALAAM
SERIKALI imesaini mikataba na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) yenye thamani ya Euro milioni 118.8 (sawa na bilioni 323.4/-) kwa ajili ya kutekeleza miradi minne ya maendeleo nchini.
Kati ya mfuko huo Euro milioni 75.9 ni mkopo wa masharti nafuu kwa awamu ya pili ya mradi wa nishati ya jua unaotekelezwa Kishapu mkoani Shinyanga.
Mradi wa Kishapu utakuwa na uwezo wa MW 150, ikiwa ni pamoja na awamu ya kwanza iliyosainiwa Juni 11, 2021 na tayari utekelezaji wake unaendelea. Awamu ya kwanza inatarajiwa kuzalisha MW 50 itakapokamilika
Mkataba wa pili ni mkopo wa masharti nafuu wa Euro milioni 39.9 kwa ajili ya mradi unaolenga kuendeleza misitu na uhifadhi wa misitu ya mikoko huku makubaliano mengine ni msaada wa Euro milioni 2 ambao ni mfuko maalum wa uhifadhi wa mikoko na makubaliano ya nne ni ruzuku ya Euro milioni 1 kugharamia mpango kazi wa jinsia wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) chini ya uendelezaji wa nishati ya jua.
ZINGATIA:- Mikataba hiyo imesainiwa Desemba 6, 2024 jijini Dar es Salaam na wizara ya Fedha na Naibu Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Axel-David Guillon na Mkurugenzi Mkazi wa AFD, Celine Robert.
