NCHI 14 ZAJA TZ KUJIFUNZA KUPUNGUZA VIFO VYA MAMA NA MTOTO
DODOMA
Serikali ya Tanzania imepokea ugeni wa wajumbe kutoka nchi 14 (Wajumbe hao ni kutoka nchi ya Ethiopia, Gambia, Lesotho, Eswatini, DRC Congo, Chad, Nigeria, Somalia, Guniea, Kenya, Uganda, Zambia, Egypt na South Sudan) zikiongozwa na Shirika la kuthibiti magonjwa Afrika (CDC Afrika) kwa lengo la kujifunza namna Serikali ya Tanzania ilivyopiga hatua kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi na watoto wachanga.
Wajumbe hao wamefanya ziara katika kituo cha Afya cha Soya kilichopo Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma Desemba 5, 2024 wakiongozwa na watendaji kutoka Wizara ya Afya Idara ya huduma za Afya ya uzazi, mama na mtoto.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo Mkuu wa Progamu ya Uzazi Salama Wizara ya Afya Dkt. Phineas Sospeter amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi chache barani Afrika zilizoweza kupunguza vifo vya wajawazito kwa kiasi kikubwa ambapo toka miaka saba iliyopita vifo vya vitokanavyo na uzazi vimepungua kutoka 556 kwa kila vizazi hai 100,000 kwa mwaka 2015/2016 na kufikia vifo 104 kwa kila vizazi hai laki moja mwaka 2022.
