DKT SAMIA AHIMIZA USALAMA BARABARANI
DAR ES SALAAM
Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ameliagiza Jeshi la Polisi kuhakikisha madereva wanaongeza umakini na kuzingatia sheria za barabarani katika kipindi hiki cha mwisho wa mwaka ili kuepusha ajali zinazoweza kuepukika.
Dkt Samia ametoa agizo hilo Desemba 4, 2024 katika taarifa yake ya kusikitishwa na taarifa za ajali iliyohusisha magari matatu katika kijiji cha Kihanga, Wilaya ya Karagwe Mkoa wa Kagera na kusababisha vifo vya watu saba na majeruhi tisa (jana)
“Ninawapa pole familia, ndugu, Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mheshimiwa Fatma Mwassa, jamaa na marafiki.
Ninawaombea kwa Mwenyezi Mungu marehemu wote wapumzike kwa amani, na majeruhi wote wapone kwa haraka,” ameandika Dkt Samia kupitia mtandao wa X.
Aidha, kiongozi huyo wa nchi amewataka abiria na watumiaji wote wa barabara kutumia namba za simu za makamanda wa polisi wa mikoa kutoa taarifa kwa jeshi la polisi wanapoona viashiria vya uzembe na ukiukwaji wa sheria na alama za barabarani.
“Utekelezaji wa agizo hili uende sambamba na uhuishaji na uwekaji wa alama za barabarani kwenye maeneo hatarishi, pamoja na kuzingatia umbali na maeneo sahihi ya uwekaji wa vituo vya ukaguzi ili vionekane kwa urahisi zaidi,” ameongeza Mhe Rais Samia.
