TSH BIL 60 KUBORESHA BANDARI ZA ZIWA VICTORIA
MWANZA
Serikali ya Tanzania imewekeza kiasi cha Shilingi bilioni 60 kwa ajili ya kuboresha bandari tatu kuu za Ziwa Victoria.
Uwekezaji huu mkubwa katika bandari za Kemondo, Bukoba na Mwanza Kaskazini unatarajiwa kuboresha ufanisi na uwezo wa huduma za usafiri katika eneo hilo.
Kazi ya kuboresha Bandari ya Kemondo, imekamilika kwa asilimia 98 na hatua za mwisho zinahusisha kusafisha eneo kabla ya kuzinduliwa rasmi na mradi wa kuboresha Bandari ya Bukoba kwa umefikia asilimia 75 ya kukamilika.
Maboresho yanayoendelea yanakusudia kuongeza kina cha maji kutoka mita 3.5 hadi mita 5 katika Bandari za Kemondo na Bukoba. Pia, mabadiliko mengine yanahusisha kuongeza urefu wa gati kutoka mita 75 hadi 92, kuboresha eneo la sakafu kwa kuimarisha muundo wa zege, na kufunga uzio wa kuimarisha usalama huku maboresho mengine yakijumuisha ujenzi wa maeneo ya kusubiri abiria, vituo vya ukaguzi wa mizigo, mfumo wa umeme wa kisasa, na kinga ya upepo.
Aidha serikali inaanzisha vituo vya huduma vya sehemu moja katika bandari zote zinazoboreshwa, ikijumuisha huduma za Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Misitu, Uhamiaji, Afya, na Wakala wa Forodha na Uondoshaji Mizigo pamoja na vikosi vya ulinzi na usalama ili kuboresha utoaji wa huduma.
Maboresho haya yanalenga kusaidia kupokea MV Mwanza Hapa Kazi Tu, meli mpya ya abiria inayojengwa na ambayo itakuwa kubwa zaidi Afrika Mashariki. MV Mwanza Hapa Kazi Tu itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 1,200, tani 400 za mizigo, magari madogo 20, na magari makubwa matatu, hivyo kuongeza maradufu uwezo wa abiria ikilinganishwa na MV Victoria inayobeba abiria 600 kwa sasa.