TANZANIA,URUSI KUIMARISHA KILIMO, UTALII
DAR ES SALAAM
Wizara ya Mipango na Uwekezaji ya Tanzania imetangaza kuwa ushirikiano mkubwa kati ya Tanzania na Urusi unatazamiwa kukuza kwa kiasi kikubwa ukuaji wa sekta ya kilimo na utalii na kuchangia maendeleo ya kiuchumi ya nchi zote mbili. Hii ni kwa mujibu wa mkutano na waandishi wa habari kufuatia kongamano la wafanyabiashara na mkutano wa kamisheni ya pamoja uliowakutanisha Prof Mkumbo na Waziri wa Maendeleo ya Uchumi wa Urusi, Maxim Reshetnkov.
Kupitia Mkutano huo mataifa hayo mawili yalijadili na kusaini makubaliano kuhusu masuala matano muhimu yanayolenga kuboresha sekta za kijamii na kiuchumi.
Miongoni mwa maeneo muhimu yaliyoshughulikiwa ni kilimo, hasa uzalishaji wa mbolea; huduma ya afya, ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa dawa na chanjo; uzalishaji wa nishati mbadala, hasa gesi, elimu, inayolenga kufundisha lugha ya Kiswahili nchini Urusi na maendeleo ya utalii.
Kuhusu utalii, mikataba hiyo inatarajia kuanzishwa kwa safari za ndege za moja kwa moja kutoka Zanzibar na Dar es Salaam hadi Moscow, hivyo kurahisisha usafiri wa watalii na bidhaa za Urusi kuja Tanzania.
Aidha Mkutano huo ulijumuisha wawakilishi wa wafanyabiashara zaidi ya 120 kutoka Urusi na serikali inapanga kuanzisha njia za moja kwa moja kati ya Moscow na Zanzibar, pamoja na Dar es Salaam.
