MRADI WA RUSUMO WAFIKIA 99.9%
KAGERA
Mradi wa Kufua Umeme wa Rusumo unaosimamiwa na nchi za Tanzania, Burundi na Rwanda utekelezaji wake umefikia asilimia 99.9 huku ukitarajiwa kuzinduliwa Februari 2025 huku ma-Rais wa nchi hizo tatu wakitarajiwa kuhudhuria hafla ya uzinduzi huo.
Mradi wa huo wa kufua umeme unaotokana na maji wa Rusumo, umeanza kuzalisha megawati 80 ambazo zinagawanywa kwa usawa wa megawati 26.66 kwa nchi ya Tanzania, Rwanda na Burundi na hivyo kuzidi kuimarisha gridi za Taifa za umeme.
Mradi huo unaotekelezwa na Kampuni ya Umeme ya Rusumo (RPCL) inayomilikiwa na nchi zote tatu ni kielelezo cha azma ya Serikali ya Tanzania kuhakikisha kuwa nchi inakuwa na umeme wa kutosha na wa uhakika kwa ajili ya shughuli za maendeleo na kijamii.
Aidha manufaa ya mradi huo hadi sasa umezalisha ajira kwa watu pamoja na kusaidia uwepo wa miradi mbalimbali kwa ajili ya huduma kwa jamii (CSR) hususan katika Halmashauri ya Ngara.
Aidha, mradi huo umeiunganisha Tanzania na nchi za Rwanda na Burundi na pia unatoa fursa ya kuziuzia umeme nchi hizo endapo zitahitaji licha ya uwepo wa megawati 26.66 zinazopatikana kwa kila nchi.
