UN YAIPONGEZA TZ KUKUZA AMANI,HAKI ZA BINADAMU,DEMOKRASIA
DAR ES SALAAM
Umoja wa Mataifa (UN) umeipongeza Tanzania kwa kuendelea kusimamia misingi yake mikuu, ikiwemo kukuza amani, haki za binadamu na demokrasia sambamba na kuharakisha utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), hii ni kwa mujibu wa kaimu mratibu wa Umoja wa Mataifa Bw. Bryan Schreiner kupitia maaadhimisho ya Miaka 79 tangu kuanzishwa kwake Oktoba 1945 yaliyofanyika katika ofisi za umoja wa Mataifa Jijini Dar Es salaam.
Bw. Bryan Schreiner ameipongeza Tanzania kwa kudumisha uhusiano wa muda mrefu na wenye kujenga, akiielezea nchi hiyo kuwa mwanachama mtukufu wa chombo hicho cha kimataifa tangu Desemba 14, 1961.
Kikubwa zaidi, aliipongeza Tanzania kwa kuendelea kuharakisha utekelezaji wa SDGs kupitia kwa kuboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi wote na kutetea usawa wa kijinsia.
Aidha, aliipongeza Tanzania kwa kuja na Mkakati wa Kitaifa wa nishati Safi ya kupikia mpango unaolenga kuhifadhi mazingira kwa kuzuia ukataji miti na uchafuzi wa mazingira unaosababishwa na upishi usio safi unaohusisha matumizi ya kuni na mkaa.
"Kwa miaka mingi, Tanzania imechangia kikamilifu katika kuunda ajenda ya maendeleo ya kimataifa," Bw Schreiner alisema.
Chini ya mkakati wa nishati safi ya kupikia, Tanzania inalenga kuhakikisha unafikia asilimia 80 ifikapo 2034 kutoka asilimia 10 ya sasa. Alikumbusha kuwa nchi hiyo ilizindua Mfumo wake wa Ushirikiano Endelevu wa Umoja wa Mataifa (UNSDCF) mwaka 2022 ili kuendana na msukumo wa kimataifa wa kufikia SDGs.
Mfumo huo ambao sasa uko katika mwaka wake wa tatu wa utekelezaji, unajumuisha dhamira ya Tanzania ya maendeleo endelevu na shirikishi. Bw Schreiner alisema tangu kupitishwa kwa UNSDCF imekuwa ikitoa mwongozo kwa Umoja wa Mataifa kuunga mkono juhudi za Tanzania katika kufikia mipango yake ya maendeleo ya kitaifa katika kutekeleza SDGs.
