DKT SAMIA AWATAKA WAKULIMA KUONGEZA UZALISHAJI
MOROGORO
Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan amewataka wakulima kote nchini kuongeza juhudi za uzalishaji wa mazao ili kuhakikisha nchi inaendelea kujitosheleza kwa chakula ikiwa ni pamoja na kuzalisha ziada kwa ajili ya kuuza nje ili kunufaika na soko lililopo.
Dkt Samia ameyasema hayo wakati akizungumza mara baada ya kuzindua hospitali ya wilaya ya Gairo Mkoani Morogoro ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi katika mkoa huo.
Dkt Samia amesema wakulima wanapaswa kuendelea kuzalisha mazao ya biashara na chakula, kwani hadi sasa yote yanazingatiwa kama mazao ya biashara.
"Ninawahimiza wakulima kuendelea kuzalisha mazao ya biashara na chakula, kwani siku hizi mazao yote yanachukuliwa kuwa mazao ya biashara. Hata mbaazi sasa ni zao la biashara, amesema.
Dkt Samia amebainisha kuwa Tanzania, kupitia juhudi za wakulima wote nchini, inaweza kujitosheleza kwa chakula kwa asilimia 120. "Tukifikia kiwango hiki, itamaanisha kuwa kila Mtanzania hakosi chakula kwa mwaka mzima, na tutakuwa na nyongeza ya asilimia 20 ya mazao yatakayouzwa nje ya nchi na tumeanza kuuza nje" ameongeza.