TIC KUVUNA TSH BIL 260 ZA JAPAN
DAR ES SAAAM
Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimejipanga kukuza uwekezaji wa Japan nchini Tanzania hadi dola za Marekani milioni 100 (takribani shilingi bilioni 260) ifikapo Desemba 2025 kutoka dola za Marekani milioni 42 za sasa (shilingi bilioni 109).
Katika taarifa iliyotolewa hivi karibuni na Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Gilead Teri amesema wawekezaji wa Japan wanaweza kuwekeza zaidi Tanzania kwa kutumia mazingira mazuri ya biashara ambayo yameainishwa na Sheria Mpya ya Uwekezaji ya 2022 iliyopitishwa na Bunge la Tanzania Chini ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan
Kwa mujibu wa TIC, Ujumbe wa kukuza uwekezaji Tanzania ulioanza Mei 26 mwaka huu nchini Japan kupitia semina na mijadala unaangazia sekta mbalimbali zikiwemo za viwanda, nishati, majengo, miundombinu, usindikaji wa mazao ya kilimo na dawa.
Aidha, TIC itatenga ardhi kwa ajili ya Japan na wawekezaji wa Tanzania kwa ajili ya kuanzisha eneo la pamoja la viwanda litakalochukua viwanda vya awali kama vile kuunganisha magari na mashine nyinginezo.
Vilevile ujumbe wa TIC Nchini Japan ambao umeenda tangu Mei na utamaliza ziara tarehe 7 Juni na hadi sasa umekutana na kampuni kubwa za Japan zikiwemo Toyota, Toppan, Fujistu, Seiko, Epson, Sumitomo, Marubeni, JGC Corporation, Tshusho na Mitsubishi Corporation.