TANZANIA, INDIA KUSHIRIKIANA (NISHATI SAFI YA KUPIKIA)

 

TANZANIA, INDIA KUSHIRIKIANA (NISHATI SAFI YA KUPIKIA)

TANZANIA, INDIA KUSHIRIKIANA (NISHATI SAFI YA KUPIKIA)

DODOMA
Serikali ya India imeahidi kushirikiana na Tanzania katika kuhakikisha lengo la utekelezaji wa mkakati wa matumizi ya nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034 linafikiwa, hatua itakayosaidia kupunguza matumizi ya kuni na mkaa na kuhamasisha uhifadhi wa mazingira.Hii ni kwa mujibu wa kikao kati ya Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Christina Mndeme na Naibu Balozi wa India nchini Tanzania, Mhe. Manoj Verma kilichofanyika katika Mji wa serikali Mtumba Mkoani Dodoma Juni 20, 2024.
Balozi Mhe. Verma amepongeza juhudi zinazoendelea kufanywa na Serikali ya Tanzania katika kuhakikisha jamii yake inahamia katika mfumo wa matumizi ya nishati safi ya kupikia hatua inayolenga kuepukana na matumizi ya nishati chafu ambayo imekuwa na madhara makubwa kwa afya ya binadamu na mazingira.
“India imepiga hatua kubwa katika matumizi ya nishati safi ya kupikia ambapo takribani asilimia 80 ya wananchi wa mijini na vijijini wanatumia nishati hiyo, Tupo tayari kushirikiana na Tanzania katika kuhakikisha ajenda hii inafikiwa kwa wananchi wake” amesema Mhe. Verma
Kuelekea kuunga mkono juhudi za Mhe Rais Dkt Samia, Mhe Verma amesema katika kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa mazingira, tarehe 5 Juni mwaka huu Serikali ya India imezindua Kampeni ya Upandaji Miti ijulikanayo “A tree for Mother” inayolenga kuhamasisha dunia umuhimu wa kupanda miti kwa ajili ya uhifadhi wa mazingira na rasilimali za viumbe hai mbalimbali, hivyo Serikali ya India imekusudia kupanda miti bilioni 1 hatua inayolenga kuhamasisha jamii kutambua umuhimu wa kulinda mazingira na uhifadhi wa baianoai mbalimbali na hivyo kufikia malengo ya maendeleo endelevu.