TSH BIL 96+KUONGEZA NGUVU MRADI WA KAKONO
KAGERA
Tanzania na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) zimetiliana saini makubaliano ya fedha ya ziada yenye thamani ya Euro milioni 34.86 (sawa na 96.47bn) kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa Umeme wa Maji wa Kakono uliopo Manispaa ya Bukoba kando ya Mto Kagera Mkoani Kagera ambao utakapokamilika utaingiza kwenye gridi ya Taifa takriban Megawati 87.8.
Lengo la mradi huo ni kuongeza uzalishaji wa nishati kwenye gridi ya taifa kwa kutumia chanzo cha gharama nafuu ambacho ni cha maji, ili kukabiliana na upungufu wa umeme Kaskazini Magharibi mwa Tanzania.
Uendelezaji wa Kiwanda cha Kufua Umeme cha Kakono (HPP) kitachukua nafasi ya matumizi ya nishati ya kisukuku Kaskazini Magharibi mwa Tanzania katika Kanda ya Ziwa, ambapo jenereta za gharama kubwa za dizeli hutumiwa ama kuongeza usambazaji wa gridi ya taifa au kuboresha ubora wa usambazaji ili kuepusha kukatika kwa umeme kwa muda mrefu
Aidha mradi huu unafadhiliwa na Washirika watatu wa Maendeleo ambao ni AFD (Euro milioni 110 sawa na takriban 304.37bn/-), Benki ya Maendeleo ya Afrika (USD 161.47 milioni sawa na takriban bilioni 413.95) na Umoja wa Ulaya (Euro 34.86 milioni, sawa na 96.47bn ) zitakazosimamiwa na AFD).
Mradi wa Umeme wa Maji wa Kakono unaenda sambamba na Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP III) wenye kaulimbiu isemayo ‘Kujenga Uchumi wa Kiushindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu kwa kuboresha miundombinu yenye tija, upatikanaji wa nishati ya uhakika, kuimarisha mazingira wezeshi ya biashara na uwekezaji. pamoja na mifumo ya elimu na mafunzo.
NB:- Mkataba uliosainiwa awali Machi 15,2023 kati ya wizara ya fedha ya Tanzania na Mashirika ya Kimataifa ya Maendeleo ulikuwa wenye thamani ya shilingi bilioni 750 za Kitanzania.
