KONGAMANO LA MUHOGO KUFANYIKA APRIL 15
DODOMA
Serikali imetaja hatua inazozichukua ikiwa ni moja ya jitihada zake za kugeuza muhogo kuwa zao la kimkakati, lenye uwezo wa kuchangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi wa nchi na moja ya hatua hizo pamoja na kufanya Jukwaa la Biashara ya Muhogo Aprili 15, 2024, jukwaa ambalo litavutia idadi kubwa ya wadau.
Katika kongamano hilo, wadau watajadili fursa zilizopo katika mikoa ya kusini kwani Muhogo ni zao la tatu kwa umuhimu wa chakula nchini Tanzania baada ya mahindi na mpunga.
Hatua zingine kuelekea ukombozi wa zao la muhogo ni pamoja na kuhamasisha matumizi ya miche bora ya muhogo iliyotengenezwa na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) yenye uwezo wa kuzalisha kati ya tani 20 na 50 kwa ekari moja.
Pia Kuelekea mpango wa kupandisha hadhi muhogo, Serikali imeandaa Mkakati wa Taifa wa Maendeleo ya Muhogo (NCDS) 2020- 2030 unaohamasisha kilimo cha zao hilo, upatikanaji wa masoko ya uhakika, na uanzishaji wa viwanda vya usindikaji vikiwemo vile vinavyoweza kuzalisha mazao ya muhogo.
Aidha matumizi ya miche iliyoboreshwa yamewezesha uzalishaji wa muhogo mkavu kutoka tani 2,486,000 msimu wa kilimo 2020/2021 hadi tani 2,575,453 msimu wa kilimo 2022/2023 huku wastani wa uzalishaji kwa mwaka ni kati ya tani 3.5 kwa hekta hadi tani 8.5 kwa hekta.
Vilevile matokeo muhimu yanayotarajiwa kutoka kwa mkakati huu yatajumuisha kuongezeka kwa uzalishaji na tija,kuongezeka kwa matumizi ya teknolojia zilizoboreshwa kwenye mnyororo wa thamani wa muhogo, kuboresha masoko ya muhogo na miundombinu inayohusiana nayo, kuongeza ajira na ukuaji wa uchumi kwa ujumla.