MIRADI YA KITAIFA INAYOTEKELEZWA RUVUMA
Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan imeendelea kutoa mabilioni ya fedha kutekeleza miradi mbalimbali ya kitaifa katika Mkoa wa Ruvuma.
1. Uwanja wa Ndege Songea
Uwanja wa Ndege wa Songea ni mojawapo ya miradi mikubwa ya kitaifa inayolenga kuboresha miundombinu ya usafiri wa anga, Mradi huu umetumia gharama ya shilingi bilioni 38.139 na umekamilika Disemba 2023.
Kukamilika kwa uwanja huu kunatarajiwa kuboresha huduma za usafiri wa anga na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika eneo hilo.
2. Barabara ya Likuyufusi-Mkayukayu
Mradi wa ujenzi wa barabara ya Likuyufusi-Mkayukayu unahusisha ujenzi wa kilometa 60 kwa kiwango cha lami. Hivi sasa, mradi huu uko katika hatua za mwisho za manunuzi baada ya mkandarasi wa awali kubainika kuwa hana uwezo wa kutekeleza kazi ipasavyo.
Serikali imetumia kais cha shilingi bilioni 5.2 kwa ajili ya kulipa fidia waliopisha ujenzi wa barabara hii
Ujenzi wa barabara hii unatarajiwa kuongeza ufanisi wa usafiri na kurahisisha shughuli za kiuchumi katika eneo hilo.
3. Barabara ya Songea-Rutukira na Songea Bypass
Huu ni mradi mkubwa wa ujenzi wa barabara ya kilomita 116, ikijumuisha kilomita 16 za barabara ya mchepuko ya Songea (Songea Bypass).
Mradi huu unafadhiliwa na Benki ya Dunia na unasimamiwa na wahandisi washauri wa kampuni za LEA International, LEA Associates na Howard and Humphrey.
Hadi hivi sasa fidia ya shilingi milioni 646.964 imeshalipwa kwa waathirika wa mradi katika sehemu ya Songea - Lutukira, huku fidia kwa barabara ya mchepuko ya Songea bado ikisubiri taratibu za mwisho za malipo.
Kukamilika kwa mradi huu kutarahisisha usafiri na kupunguza msongamano wa magari mjini Songea.
4. Barabara ya Lumecha-Kilosa-Kidatu
Mradi huu unahusisha ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilomita 435.8 kwa kiwango cha lami, ambayo itaunganisha Mkoa wa Ruvuma na Morogoro.
Awali, mradi huu ulikuwa umepangwa kutekelezwa kwa mtindo wa Usanifu, Manunuzi, Ujenzi na Ufadhili, lakini sasa utafuata mtindo wa Sanifu na Jenga (Design and Build).
Ujenzi wa barabara hii unatarajiwa kuimarisha usafiri kati ya mikoa hiyo miwili na kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa kuongeza kasi ya usafirishaji wa bidhaa na abiria.
Miradi hii yote ni sehemu ya juhudi za serikali kuboresha miundombinu ya usafiri na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini. Kukamilika kwake kutakuwa na mchango mkubwa katika kurahisisha usafiri, biashara na uwekezaji