TSH TRIL 13+ ZA MATTEI KUINUFAISHA TANZANIA
ITALIA
Tanzania imechaguliwa kuwa moja ya nchi nane za Afrika zitakazopewa kipaumbele na Italia kupitia mpango mpya wa kimkakati wa Mattei (Mattei Plan) ambapo kiasi cha Euro bilioni 5 za awali (sawa na shilingi 13,915,421,864,590.84 za kitanzania) kimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo
Miradi hiyo ya kipaumbele kupitia Mpango mpya wa Kimkakati wa Mattei (Mattei plan) ipo katika sekta ya nishati, elimu na kilimo
Chanzo:- Rais wa Chama cha Wafanyabiashara wa Italia, Mhandisi Alfredo Cestari alipokutana na wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (Tanzania) pembezoni mwa Mkutano wa Nne wa Wakuu wa Nchi za Afrika na Italia uliofanyika Roma, Italia.
Mhandisi Cestari ameeleza kuwa utekelezaji wa mpango huo utaanza mara baada ya kumalizika kwa mkutano wa Wakuu wa nchi za Afrika na Italia, ambapo Serikali ya nchi hiyo itafadhili miradi ya kipaumbele kwa nchi nane za awali za Afrika. Hatua hiyo itahusisha pia kugharamia gharama za upembuzi yakinifu ya miradi itakayopendekezwa.
Kama hatua ya utekelezaji ya mpango huo, ujumbe wa wataalam kutoka Chemba ya Biashara ya Italia ikiongozwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia, Dkt. Edmondo Cirielli unatarajiwa kuwasili nchini Tanzania ndani ya mwezi mmoja kwa ajili ya kukutana na timu ya wataalam upande wa Tanzania kwa ajili ya kukamilisha hatua za awali za utiaji saini wa ushirikiano huo wa pande mbili utakaohusisha utekelezaji wa miradi itakayopitishwa na pande mbili.
Pamoja na mambo mengine, mkutano huo umelenga kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ili kuongeza kiwango cha biashara na uwekezaji baina ya mataifa hayo mawili kupitia mpango mpya wa Mattei, (Mattei Plan)
