TSH MIL 688 KUZINUFAISHA MWANZA, IRINGA NA KAGERA
DAR ES SALAAM,
Mikoa mitatu ya Tanzania (Mwanza, Iringa na Kagera) imenufaika na kiasi cha milioni 688 kutoka serikali ya Japan, fedha zilizotolewa kwa ajili kutekeleza Miradi ya Msingi ya Usalama wa Binadamu (Grassroots and Human Security Project GGHSP)
Fedha hizo zimeelekezwa katika kuimarisha elimu na kuboresha vituo vya afya katika ngazi ya chini, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa shule, zahanati na utoaji wa vifaa vinavyohusika.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini huo jijini Dar es Salaam,Balozi wa Japan nchini, Yasushi Misawa, amesema
“Tumesaini mkataba wa ujenzi wa mabweni ya wasichana katika Shule ya Sekondari Kagera, Zahanati ya Malagosi mkoani Iringa na ujenzi wa jengo la afya ya uzazi na mtoto katika Hospitali ya Wilaya ya Sumve, Mwanza".
Balozi Misawa ameongeza kuwa miradi hiyo inaashiria hatua muhimu ya kuimarisha ushirikiano kati ya Japan na Tanzania.
Mradi huo ulioanzishwa na Serikali ya Japani mwaka wa 1989, Grassroots and Human Security Project (GGHSP) unafuata kanuni ya ‘Usalama wa Binadamu,’ iliyoanzishwa na aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Kuhudumia Wakimbizi, Bibi Sadako Ogata.
