TSH MIL 528 ZAWAOKOA WATOTO KUTEMBEA KM 21
MOROGORO
Wananchi wa Kijiji cha Ruhembe, Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro wameonesha furaha yao baada ya serikali kutoa kiasi cha shilingi milioni 528 kwa ajili ya kujenga shule mpya ya sekondari Miwa kupitia mradi wa Kuboresha Elimu ya Sekondari (SEQUIP).
Mwenyekiti wa Kijiji cha Ruhembe Abdallah Kambi amesema "Kiukweli kwa sasa wananchi hatuna adha tena ya shule ya sekondari katika hiki kijiji tunamshukuru sana Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kupambana kuwekeza miradi ya elimu."
Ameongeza kwamba hapo awali watoto wa kijiji hicho walikuwa wanapata changamoto ya kwenda shule umbali wa kilomita 21 sababu ikiwa ni umbali na makazi na jiografia ya kijiji hicho kimezungukwa na mashamba ya miwa maeneo mengi yanaonekana ni pori,ambapo watoto walikuwa wanakumbana na matukio mengi na hasa kwa watoto wa kike kufanyiwa vitendo vya kikatili.
Ameongezea kwa kusema watoto hao ( hasa wa kike) walikuwa wanashindwa kumaliza shule sababu ya changamoto zikiwemo za umbali wa shule waliokuwa wanaenda, kufanyiwa vitendo visivyofaa kama kubakwa, kupata ujauzito na mambo mengine ambayo yalikuwa ni changamoto kwa watoto hao wakike.
Naye mkazi wa Kijiji hicho Fitina Nganywela amesema uwepo wa shule hiyo imewasaidia pia wao kama wazazi kuwa na imani na watoto wao sababu shule hiyo ipo karibu na maeneo ya makazi ambapo ni rahisi hata kwa mzazi kumfuatilia mtoto maendeleo yake shuleni na mwenendo mzima wa elimu.