DKT SAMIA ATAKA USIMAMIZI MZURI WA FEDHA ZA MIRADI.
DAR ES SALAAM
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Rais Samia Suluhu Hassan amewataka wakuu wa mikoa kusimamia kwa weledi fedha zinazopelekwa katika maeneo yao ya kazi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Akizungumza kwenye hafla ya uapisho wa viongozi mbalimbali wateule Mhe Rais amesema
"Fedha nyingi zinashushwa kwenda chini, madhumuni ya fedha hizo kushushwa sio kwenda kuliwa, ni kwenda kutatua changamoto za wananchi"
Aidha Mhe Rais Dkt Samia amesisitiza kuhusu usimamizi wa ukusanyaji wa mapato kwa Halmashauri ambazo zinakusanya chini ya 50%
"Wale wa chini ya 50%mnajijua, kajitazameni mjue wapi mtakusanya,lakini katika kupandisha makusanyo sio kwenda kuwaonea wananchi,sio kuwabinya wananchi,kuna maeneo mengi ya fedha ambazo mmeziachia zinapita,watu wengine wanazidaka, kajiangalieni upya ni wapi mnaweza kukusanya bila kuleta usumbufu kwa wananchi" Amesema Dkt Samia.
Hafla ya kuwaapisha Viongozi wateule imefanyika leo tarehe 13 Machi, 2024 katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Ikulu jijini Dar es Salaam.
