TANZANI NAMBA 1 ULINZI WA MTANDAO

 

TANZANI NAMBA 1 ULINZI  WA MTANDAO

TANZANI NAMBA 1 ULINZI  WA MTANDAO

ARUSHA
Tanzania imeorodheshwa Daraja la Kwanza miongoni mwa nchi 46 duniani zinazofanya vizuri katika masuala ya ulinzi wa kimtandao, hii ni kwa mujibu wa ripoti ya kimataifa ya masuala ya kimtandao (GCI) 2024 iliyosomwa na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA nchini (ICTC), Dk Nkundwe Mwasaga wakati akifungua Jukwaa la Nne la Usalama wa Kimtandao la Tanzania 2025 jijini Arusha.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Tanzania imejikita katika nguzo kuu tano ili kufikia mageuzi makubwa ya kidijitali ikiwemo kukuza ujuzi wa kidijitali, usalama na uaminifu katika masuala ya kidijitali, huduma za mawasiliano ya kidijitali, kujenga uchumi wa kidijitali, kufanya tafiti za kidijitali, ubunifu na ujasiriamali katika masuala ya kidijitali.
kutokana na nguzo hizo tano, Tanzania imeanza kupata mabadiliko chanya katika masuala ya kidijitali na usalama wa kimtandao ikiwemo kutumia na kufaidika na teknolojia na majukwaa ya kidijitali kuufanya uchumi wa Tanzania kuwa wa ushindani zaidi.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kila ukanda duniani una nchi ambazo ni mfano wa kuigwa au zinazoendelea, na kila ukanda una nchi ambazo ziko katika hatua za mwanzo za kujenga usalama wa mtandao.
Naye Kamishna wa Ulinzi wa Taarifa za Mtandaoni kutoka Ujerumani, Dk Tino Nauman amesema, anatambua Tanzania ina sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi kama ilivyo Ujerumani na nchi nyingine ambalo ni jambo muhimu kwa maendeleo ya uchumi wa kidijitali.
Ameongeza, taarifa yoyote inayomhusu mtu binafsi, kisheria hiyo ni taarifa binafsi kama vile umri wa mtu au namba ya utambuzi, mawasiliano ya mtu na mtu, barua pepe na mengineyo.