TSH BIL 14+ KUSAMBAZA UMEME VITONGOJINI PWANI
PWANI
Serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imetoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi wa Kusambaza umeme kwenye vitongoji 135 katika mkoa wa Pwani, mradi ambao utatekelezwa na Mkandarasi kampuni ya China Railway Construction Electrification Bureau Group Co. Ltd kutoka Nchini China.
Mkoa wa Pwani una jumla ya vijiji 417 ambapo vijiji 407 sawa na asilimia 98 vimeunganishwa na umeme na vijiji 10 ambavyo havijafikishiwa umeme vipo kwenye maeneo ya delta katika Wilaya ya Kibiti (vijiji 5) na visiwa katika Wilaya ya Mkuranga (vijiji 3) na Mafia (vijiji 2) ambapo tayari mpango umeandaliwa na vitafikishiwa umeme wa nishati mbadala kupitia miradi ya off-grid.
Kwa upande wa vitongoji, Mkoa wa Pwani unajumla ya vitongoji 2,045 ambapo hadi sasa vitongoji 1,135 vimepata huduma ya umeme mbayo ni sawa na asilimia 55.6 hivyo mkandarasi atatekeleza mradi katika vitongoji 135 ikiwa na maana vitongoji 15 kwa kila jimbo katika majimbo yote tisa ya Mkoa wa Pwani kwa gharama ya shilingi 14,983,763,390.
Aidha vitongoji 775 vilivyobaki vitaendelea kupatiwa umeme kulingana na upatikanaji wa fedha.